
Klabu ya TP Mazembe inaposherehekea kutwaa ubingwa wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, Wanzania wana kila sababu ya kujionea fahari hata zaidi.
Mmoja wao, Mbwana Ally Samatta, alichangia sana katika ushindi huo.
Mshambuliaji huyo amekuwa akiwika sana na baada ya kufunga penalti wakati wa ushindi wao wa 2-0 dhidi ya USM Alger ya Algeria Jumapili, amemaliza akishikilia nafasi ya ufungaji mabao mengi zaidi ligi hiyo mwaka huu pamoja na Bakry 'Al Medina' Babiker wa Al Merrikh ya Sudan.
Wawili hao wamefunga mabao saba msimu huu.
Ushindi wa Mazembe unawatwisha jukumu la kuwakilisha bara la Afrika katika Kombe la Dunia la Klabu mwezi ujao nchini Japan, ambako bila shaka Samatta atakuwa na fursa nzuri ya kujitangaza kwa ulimwengu.
Ndoto yake ni kucheza ligi za soka Uingereza, na nyota ya jaha ikiendelea kumuangazia atatua huko karibuni.
“Sijaelewa ni kwa nini hatuna wachezaji Ulaya lakini nina uhakika ninaweza kuwa mmoja,” aliambia Tanzania kumekucha awali.
Lakini alisema anajionea fahari sana kugonga vichwa vya habari na kuwakilisha taifa lake.
"Kabla nifike hapa, si watu wengi walijua kuhusu soka ya Tanzania lakini hilo linabadilika sasa. Kama taifa, hatuna wachezaji wengi wanaocheza soka ng’ambo kwa hivyo unapochezea timu kubwa kama Mazembe, kila mtu anakuona,” alisema.
Ni Watanzania wawili pekee waliowali kucheza soka ligi za juu Ulaya.
Mwaka 2010, Haruna Moshi aliondoka klabu ya ligi kuu ya Sweden Gefle IF baada ya kushindwa kung’aa, ilhali Renatus Njohole alifana akichezea klabu ya ligi kuu ya Uswisi Yverdon Sport kati ya 1999 na 2001.
Samatta wakati mmoja alihusishwa na kuhamia Spartak Moscow ya Urusi na nusura aenda Lille ya Ufaransa kwa mkopo lakini hilo halikuwa.

Ingawa azma yake ni kufika Ulaya, anasema anataka kuhakikisha anaendelea kung’aa akichezea Mazembe na timu ya taifa ya Tanzania.
Samatta ana umri wa miaka 23 na alizaliwa jijini Dar es Salaam.
Alijiunga na Mazembe kutoka klabu ya Simba ya Dar es Salaam miaka minne iliyopita.
Awali, aliichezea Africa Lyon FC ya Dar es Salaam aliyojiunga nayo mwaka 2008 kabla ya kuhamia Simba 2010.
Samatta alishinda ubingwa wa ligi kuu Congo 2011, 2012, 2013, 2014 akiwa na TP Mazembe.
Aidha, alifika nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara tatu mwaka 2012, 2014 na mwaka huu ambao hatimaye wameondoka na ubingwa.
Samatta alitambulika na klabu yake ya TP Mazembe kwa kutunukiwa mchezaji bora wa klabu mwaka wa 2013.
Kijana huyo ni miongoni mwa wachezaji wachezaji 24 walioteuliwa kuwania tuzo ya mchezaji bora Afrika anayecheza ligi ya barani Afrika mwaka huu.
Chapisha Maoni